Hamia kwenye habari

APRILI 6, 2016
HUNGARIA

Bamba la Kuwakumbuka Mashahidi Waliouawa na Wanazi Lazinduliwa Nchini Hungaria

Bamba la Kuwakumbuka Mashahidi Waliouawa na Wanazi Lazinduliwa Nchini Hungaria

BUDAPEST, Hungaria—Kituo cha Makumbusho cha Yale Maangamizi Makubwa ya Wanazi cha Budapest kimezindua bamba kwa ajili ya kuwakumbuka Mashahidi wanne wa Yehova waliosimama imara wakati wa mateso ya Wanazi. Uzinduzi huo ulifanyika Desemba 11, 2015.

Bamba la kuwakumbuka Mashahidi wanne wa Yehova waliouawa na Wanazi wakati wa Vita vya Pili vya Ulimwengu.

Wanaume hao wanne, Lajos Deli, Antal Hönisch, Bertalan Szabό, na János Zsondor waliuawa hadharani na chama cha Hungarian Arrow Cross Nazi Party mnamo Machi 1945 katika majiji ya Hungaria ya Körmend na Sárvár, kwa sababu ya kukataa kujiunga na jeshi wakati wa Vita vya Pili vya Ulimwengu. Bamba hilo limeandikwa majina yao pamoja na maneno yanayopatikana katika Biblia kwenye Matendo 5:29, “Lazima tumtii Mungu kuwa mtawala kuliko wanadamu.”

Dkt. Csaba Latorcai, katibu msaidizi wa taifa anayeshughulikia masuala ya kijamii nchini Hungaria, akitoa hotuba wakati wa sherehe ya uzinduzi.

Dkt. Csaba Latorcai, katibu-msaidizi wa taifa anayeshughulikia masuala ya kijamii, alisema hivi katika hotuba yake ya ufunguzi: “Bamba hili ni kwa ajili ya kuwakumbuka wanaume wanne ambao ni Mashahidi wa Yehova, . . . wakiwa Mashahidi wa Yehova, wao walitii ile amri isemayo ‘usiue’ na walitii dhamiri zao kwa kukataa kubeba silaha ili kuwaua waabudu wenzao au wanadamu wengine.”

Msemaji mwingine katika maadhimisho hayo alikuwa ni Dkt. Szabolcs Szita, mkurugenzi wa Kituo cha Makumbusho cha Yale Maangamizi Makubwa ya Wanazi ambaye alisema hivi: “Kuzinduliwa kwa bamba hili ni ushindi kwa sababu kwa miaka mingi Mashahidi wa Yehova wamekuwa kikundi kilichosahaulika miongoni mwa watu walioteseka wakati wa utawala wa Wanazi. Wanaume hao wanne walikuwa na imani yenye nguvu ya kudumisha azimio lao licha ya kukabili kifo. Kwa hakika wao ni mfano mzuri kwetu leo.”

Dkt. Szabolcs Szita, mkurugenzi wa Kituo cha Makumbusho cha Yale Maangamizi Makubwa ya Wanazi cha Budapest, akizindua bamba hilo.

Wanahabari wanaweza kuwasiliana na:

David A. Semonian, Ofisi ya Habari za Umma, simu +1 718 560 5000

Hungaria: András Simon, simu +36 1 401 1118