Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Rekebisha Gari Lako Bila Kujiumiza

Rekebisha Gari Lako Bila Kujiumiza

Rekebisha Gari Lako Bila Kujiumiza

Kevin alijua kubadilisha mafuta ya gari lake. Alijua kuondoa kifuniko cha mafuta, kuondoa mafuta machafu kwenye injini, na kurudisha kifuniko cha mafuta na kukikaza. Lakini wakati mmoja alipokuwa anakaza bolti, spana iliteleza. Mkono wa Kevin ulikatwa na kipande kikali cha chuma, akaumia vibaya hivi kwamba alihitaji kushonwa.

KAMA Kevin, watu wengi hujirekebishia magari yao mara kwa mara. Wengine hufanya hivyo ili kupunguza gharama. Hata hivyo, kuna faida nyingine za kujua mambo ya msingi kuhusu kutunza na kurekebisha magari. Mwanamke anayeitwa Kathy anasema: “Siku moja nilipokuwa katika safari ndefu, gari langu liliharibika. Kwa sababu nilikuwa nimejifunza kurekebisha gari, nilitatua tatizo hilo mwenyewe na kuendelea na safari.”

Labda hata wewe ungependa kujua jinsi ya kutunza na kurekebisha gari lako. Lakini unawezaje kufanya hivyo bila kujiumiza?

Jitayarishe!

Unapaswa kufikiria usalama kwanza. * Kama vile Kevin alivyoumia, ni rahisi kujiumiza unapofanya kazi mahali ambapo vitu vimerundamana au unapotumia kifaa fulani kwa nguvu. Unawezaje kuepuka kujiumiza? Unapokaza bolti, hakikisha bolti imenaswa vizuri na spana. Jiulize, ‘Kifaa hicho kikiteleza, mkono wangu utaelekea wapi?’ Unaweza kujilinda kwa kadiri fulani ukivaa glavu au ukifunga mkono wako kwa kitambaa. Ikiwezekana, elekeza kifaa hicho upande wako badala ya kukisukuma mbali nawe ili uweze kudhibiti nguvu unazotumia. Vivyo hivyo, unapolegeza bolti iliyokazwa sana, unapaswa kuilegeza kidogo-kidogo. Kanuni hizo ni muhimu nyakati zote. Usizipuuze kamwe kwa sababu ya haraka!

Mara nyingi mtu huumia anapojaribu kutumia kifaa kisichofaa kazi fulani. Kwa mfano, Tom alishindwa kubadilisha plagi za gari lake. Kwa nini? Kwa sababu shimo la spana lilikuwa dogo sana, na iliteleza mara nyingi kwenye plagi ya kwanza. Baadaye, Tom aliirefusha. Kisha akabadilisha plagi tano zilizobaki kwa muda uleule aliotumia kubadilisha plagi ya kwanza, na alifanya hivyo bila kujiumiza! Tunajifunza nini? Ni muhimu kutumia kifaa kinachofaa.

Vitu vinaweza kuingia ndani ya macho unapofanya kazi chini ya gari au ukitazama chini ya dashibodi. Unaweza kufanya nini kuzuia jambo hilo? Sean, ambaye amekuwa fundi wa gari kwa zaidi ya miaka kumi, anasema: “Linda macho yako kwa kifaa fulani, kama miwani.” Anaongezea hivi: “Kazini kwetu, ni lazima tutumie vifaa hivyo vya usalama.” Pia unapaswa kulinda macho unapofanya kazi karibu na kemikali hatari kama vile asidi ya betri.

Unapofanya kazi chini ya gari, sikuzote tumia jeki nzuri, kinara cha kuinua gari kilichotengenezwa vizuri, au uwe katika shimo imara la kutengenezea gari. Usiende chini ya gari ikiwa limeinuliwa kwa jeki pekee. Miongozo fulani kuhusu magari inaonyesha mahali ambapo jeki na vinara vinapaswa kuwekwa ili kushikilia gari vizuri. Hata hivyo unapaswa kufahamu kwamba unapolitikisa gari, labda ukijaribu kufungua bolti iliyokazika, linaweza kusonga au kuondoka kwenye jeki.

Epuka Hatari

Sehemu fulani za gari lako zinaweza kuwa moto sana na kukuunguza unapozigusa. Kwa mfano, maji kwenye rejeta (radiator) huendelea kuwa moto kwa muda fulani hata gari linapozimwa. Kwa hiyo usiondoe kifuniko mpaka kipoe ili uweze kukifungua kwa mikono. Katika magari fulani, feni ya rejeta huendeshwa kwa umeme na hufanya kazi hata baada ya injini kuzimwa. Kabla hujaanza kazi yako, ondoa waya unaounganisha umeme na ardhi kutoka kwenye betri ili usiumie.

Unaporekebisha gari, vua pete na vito vingine hasa ikiwa gari limewaka. Mbali na kugusa sehemu zilizojitokeza, vito vya chuma vinaweza kusababisha shoti ya umeme na kuwa moto sana! Nguo zinazoning’inia kama vile tai, vitambaa, na hata nywele ndefu zinaweza kushikwa na sehemu zinazozunguka.

Hata ukifikiri kwamba umemaliza kazi, kuna jambo jingine unalopaswa kuzingatia. Dirk, mshauri katika gereji moja yenye shughuli nyingi, anasema: “Sikuzote chunguza kazi yako tena. Siku moja, fundi mmoja alisahau kufanya hivyo baada ya kurekebisha breki. Basi, breki zilishindwa kufanya kazi na gari likagonga dawati langu!”

Kushughulikia Hali za Dharura

Siku moja Tom aligundua kwamba gari lake lilikuwa na joto kupita kiasi. Mrija mmoja ulikuwa umepasuka na rejeta ikamwaga maji. Tom alifunga mrija huo kwa kutumia utepe maalumu ambao alikuwa amebeba kwenye gari, akaongeza maji na maji maalumu ya kuzuia mgando. Kisha, akanunua mrija mpya. Kisa cha Tom kinaonyesha umuhimu wa kujitayarisha kwa kubeba vifaa vya urekebishaji ndani ya gari.

Unapoendesha gari, sikiliza sauti au harufu zisizo za kawaida. Yvonne alisikia harufu isiyo ya kawaida ikitoka kwenye injini ya gari lake. Mume wake alifungua boneti na kuona maji yakitoka kwenye shimo dogo katika sehemu ya juu ya mrija wa rejeta. Kwa kuwa tatizo hilo liligunduliwa kabla gari halijawa moto sana, Yvonne na mumewe waliweza kuliendesha mpaka kwenye gereji.

Ufanye nini gari lako likiharibika kwenye barabara? Kwanza, jaribu kuliweka kando ya barabara kabisa. Abiria, hasa watoto, wanapaswa kubaki ndani huku wakiwa wamejifunga kanda za usalama. Ukilazimika kuwa nje ya gari, simama mbali na magari iwezekanavyo. Washa taa za dharura. Acha boneti ikiwa imefunguka ili kuonyesha kwamba gari lako limeharibika. Weka ishara za kuonya vizuri.

Ikiwa betri imekwisha, unaweza kuiwasha ukitumia gari lingine. Lakini kumbuka kwamba betri za magari hutoa gesi inayoshika moto haraka. Cheche inaweza kuwasha gesi hiyo na kusababisha mlipuko unaoweza kukumwagia asidi kali. Kwa hiyo, ikiwa wewe au yule anayekusaidia hajui kuwasha betri, ombeni msaada.

Kama tulivyoona, kudumisha gari si mchezo. Iwe unarekebisha gari lako wakati wa dharura au ili kulitunza tu, sikuzote kumbuka: Ni lazima uzingatie usalama!

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 6 Ikiwa unarekebisha sehemu fulani kwa mara ya kwanza jitahidi upate kitabu cha mwongozo cha gari lako au umwombe rafiki mwenye ujuzi akusaidie. Iwapo gari lako lina mfumo wa kompyuta au mifumo mingine ya hali ya juu, afadhali ulipeleke kwa fundi ambaye ana vifaa vinavyofaa na uzoefu wa kurekebisha magari.

[Blabu katika ukurasa wa 21]

Mara nyingi mtu huumia anapojaribu kutumia kifaa kisichofaa kazi fulani

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 19]

Vitu Unavyopaswa Kuweka Ndani ya Gari

Gurudumu la ziada na jeki

Kebo za kuwashia betri

Ishara za kuonya

Vifaa na miwani

Tochi

Vyombo vya ziada (vya mafuta, maji, mafuta ya breki, na maji ya kupunguza mgando)

Utepe maalumu

Fyuzi

Kamba ya kuvuta gari (Kumbuka: Katika sehemu fulani sheria inaruhusu tu kampuni zenye leseni kuvuta magari yaliyoharibika)

Panga sanduku la vifaa vizuri na usimamishe vyombo

Unaweza kubeba vifaa vya ziada. Hata hivyo, mashirika fulani ya magari ambayo hutoa huduma za dharura hukataa kurekebisha gari ikiwa mwenyewe tayari ameanza kulirekebisha. Iwapo wewe ni mwanachama, waulize wanaruhusu wenye magari kufanya marekebisho gani.