Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Aleksanda wa Sita Papa Asiyesahauliwa na Roma

Aleksanda wa Sita Papa Asiyesahauliwa na Roma

Aleksanda wa Sita Papa Asiyesahauliwa na Roma

“KULINGANA na msimamo wa Wakatoliki, hakuna maneno yanayoweza kueleza kikamili lawama dhidi ya Aleksanda wa Sita.” (Geschichte der Päpste seit dem Ausgang des Mittelalters [Historia ya Mapapa Tangu Mwisho wa Enzi za Kati]) “Hakuna anayeweza kutetea maisha yake ya faragha . . . Tunapaswa kukiri kwamba cheo cha papa huyo hakileti heshima kwa Kanisa. Ingawa watu walioishi wakati mmoja na familia ya Borgia walizoea kuona matendo yenye kuchukiza, walishuhudia uhalifu wenye kutisha sana wa familia hiyo, ambao matokeo yake mabaya yamedumu hata baada ya miaka zaidi ya 400.”—L’Église et la Renaissance (1449-1517) (Kanisa na Kipindi cha Mwamko wa Elimu na Maarifa).

Kwa nini utafiti wa kihistoria uliofanywa kuhusu Kanisa Katoliki unamshutumu papa huyo na familia yake? Walifanya nini ili washutumiwe hivyo? Maonyesho yaliyofanywa huko Roma (Oktoba 2002–Februari 2003), yenye kichwa I Borgia—l’arte del potere (Familia ya Borgia—Mbinu ya Kujipatia Mamlaka), yaliwapa wahudhuriaji nafasi ya kufikiria mamlaka ya papa, hasa jinsi Rodrigo Borgia, au Aleksanda wa Sita (papa 1492-1503) alivyotumia mamlaka hayo.

Kupata Mamlaka

Rodrigo Borgia alizaliwa mwaka wa 1431 katika familia mashuhuri huko Játiva, katika ufalme wa Aragon, ambao sasa ni Hispania. Mjomba wake Alfonso de Borgia, askofu wa Valencia, alimsomesha mpwa wake wa kiume na kuhakikisha kwamba Rodrigo alipokuwa bado tineja amepewa cheo cha kidini (cheo cha kidini chenye mshahara). Alipokuwa na umri wa miaka 18, chini ya uongozi wa Alfonso, ambaye wakati huo alikuwa kadinali, Rodrigo alihamia Italia ambapo alisomea taaluma ya sheria. Alfonso alipokuwa Papa Calixtus wa Tatu, aliwafanya Rodrigo na mpwa wake mwingine wa kiume kuwa makadinali. Pere Lluís Borgia alifanywa kuwa gavana wa majiji mbalimbali. Muda mfupi baadaye, Rodrigo aliteuliwa kuwa makamu mkuu wa kanisa, cheo alichokuwa nacho chini ya uongozi wa mapapa mbalimbali. Cheo hicho kilimwezesha kupata mshahara mkubwa, kujirundikia mali, kuwa na mamlaka kubwa, na kuishi maisha ya anasa kama mwana-mfalme.

Rodrigo alikuwa mwenye akili, msemaji mwenye ufasaha, mfadhili wa sanaa, na alikuwa na uwezo wa kutimiza miradi yake. Hata hivyo, alikuwa na uhusiano haramu, akawa baba wa watoto wanne aliozaa na kimada wake na watoto zaidi aliozaa na wanawake wengine. Ingawa Rodrigo alikaripiwa na papa Pius wa Pili kwa sababu ya mwelekeo wake kuhusu “mwenendo mlegevu kingono” viburudisho vya kuchekesha na “raha zisizozuilika,” hakubadili mwenendo wake.

Papa Innocent wa Nane alipokufa mwaka wa 1492, makadinali wa kanisa walikutana ili kuchagua atakayechukua nafasi yake. Ni wazi kwamba Rodrigo Borgia aliwaahidi makadinali wengine kwamba atawalipa wakimchagua kuwa Papa Aleksanda wa Sita. Aliwalipaje makadinali waliompigia kura? Kwa kuwapa vyeo vya kanisa, majumba ya kifalme, majumba ya kifahari, majiji, makao ya watawa, na majimbo ya maaskofu ambako wangepata mishahara minono. Unaweza kuelewa sababu iliyofanya mwanahistoria mmoja wa masuala ya kanisa autaje utawala wa Aleksanda wa Sita kuwa “siku ambazo Kanisa Katoliki lilipata aibu na kashfa.”

Hakuwa Bora Kuliko Watawala wa Kisiasa

Kwa kuwa alikuwa na mamlaka ya kidini akiwa kiongozi wa kanisa, Aleksanda wa Sita alisaidia kusuluhisha mgawanyiko kati ya Hispania na Ureno uliosababishwa na kugunduliwa kwa maeneo mapya huko Amerika. Uwezo wake wa kisiasa ulifanya awe mkuu wa majimbo ya kipapa ambayo yalikuwa na maeneo katikati mwa Italia, na alitawala sawa na mtawala yeyote aliyeishi katika kipindi cha Mwamko wa Elimu na Maarifa. Utawala wa Aleksanda wa Sita sawa na ule wa mapapa waliomtangulia na wa baadaye, ulijulikana kwa hongo, kupendelea watu wa jamaa, na angalau kushukiwa kwa mauaji kadhaa.

Mataifa yenye nguvu yalikuwa yaking’ang’ania maeneo ya Italia wakati huo wenye msukosuko, naye papa huyo alishiriki kwa bidii katika pambano hilo. Mbinu za kisiasa na mapatano aliyofanya na kuyavunja, yalikusudiwa kuzidisha mamlaka yake, kuwatafutia watoto wake kazi bora maishani, na kufanya familia ya Borgia kuwa mashuhuri kuliko familia zote. Mtoto wake wa kiume Juan aliyeoa binamu wa mfalme wa Castile, alifanywa kuwa mtawala wa Gandía, Hispania. Mwana wake mwingine wa kiume aliyeitwa Jofré, alioa mjukuu wa mfalme wa Naples.

Papa alipotaka kufanya mapatano ili kuimarisha uhusiano wake na Ufaransa, alivunja uchumba kati ya binti yake Lucrezia mwenye umri wa miaka 13, na tajiri fulani wa Aragon na badala yake akamposa kwa mtu wa jamaa ya mfalme wa Milan. Alipoona kwamba ndoa hiyo haitamfaidi kisiasa, alitafuta kisababu cha kuivunja naye Lucrezia akaolewa na Alfonso wa Aragon, mshiriki wa ukoo mwingine wa kifalme wa upinzani. Wakati huohuo, ndugu ya Lucrezia, Cesare Borgia, mwenye kujitakia makuu na asiye na huruma alifanya mapatano na mfalme Louis wa Kumi na Mbili wa Ufaransa, na ndoa kati ya dada yake na Alfonso iliyokuwa imefungwa kwa muda usio mrefu ikawa yenye kuaibisha. Suluhisho likawa nini? Chanzo fulani cha habari kinasema kwamba kwa kusikitisha, Alfonso, mume wake “alijeruhiwa na watu wanne waliotaka kumwua akiwa kwenye ngazi za Kanisa la St. Peter’s. Alipokuwa anaendelea kupata nafuu, alinyongwa na mmoja wa watumishi wa Cesare.” Papa huyo ambaye alitaka kutumia mbinu mpya za kufanya mapatano, alipanga ndoa ya tatu ya Lucrezia ambaye sasa alikuwa mwenye umri wa miaka 21, ili aolewe na mwana wa mfalme mwenye mamlaka wa Ferrara.

Njia ya Cesare ya kujipatia riziki imetajwa kuwa “yenye ufisadi, iliyojaa umwagaji damu.” Ingawa baba yake alimweka rasmi Cesare kuwa kadinali akiwa na umri wa miaka 17, alifaa zaidi kwa vita kuliko kushughulikia masuala ya kanisa, kwani alikuwa mwerevu, mwenye kujitakia makuu, na mwenye ufisadi kama baadhi yao walivyokuwa. Alipoacha cheo cha kanisa, alioa binti-mfalme wa Ufaransa, na hivyo akatwaa eneo lililotawaliwa na mtawala wa Valentinois. Akisaidiwa na majeshi ya Ufaransa, Cesare alianzisha kampeni ya mazingiwa na mauaji ili kutwaa sehemu ya kaskazini ya Italia.

Ili Cesare apate msaada wa kijeshi aliohitaji kutoka Ufaransa na hivyo kuendeleza miradi yake, papa alikubaliana na talaka yenye kuaibisha lakini ambayo ingemnufaisha. Talaka hiyo iliyoombwa na Louis wa Kumi na Mbili wa Ufaransa ilimwezesha kuoa Anne wa Brittany na hivyo kupanua eneo la utawala wake. Kwa kweli, kitabu kimoja cha kitaalamu kinasema kwamba papa “alidhabihu sifa na kanuni za Kanisa ili kuwanufaisha washiriki wa familia yake kwa njia ya kisiasa.”

Papa Achambuliwa kwa Mwenendo Wake Unaopita Kiasi

Familia ya Borgia ilikuwa na maadui wengi na ilichambuliwa kwa sababu ya mwenendo wao uliopita kiasi. Papa aliwapuuza wachambuzi wake, lakini hakuweza kumpuuza Girolamo Savonarola. Alikuwa mtawa wa Dominika, mhubiri mkali, na kiongozi wa kisiasa wa Florence. Alishutumu mazoea mabaya ya mahakama ya kipapa na vilevile papa mwenyewe, matendo na siasa zake, na kutoa mwito aondolewe na marekebisho ya kanisa yafanywe. Savonarola alifoka hivi kwa hasira: “Usiku viongozi wa kanisa, . . . mnaenda kuwaona mahawara wenu kisha asubuhi mnaenda kula sakramenti.” Baadaye alisema: “[Viongozi hao] wanafanana na kahaba, umashuhuri wao unalidhuru Kanisa. Nawaambia, watu hawa hawana imani ya Kikristo.”

Ili kujaribu kumnyamazisha, papa aliahidi kumfanya Savonarola kuwa kadinali, lakini alikataa. Iwe maangamizi yake yalisababishwa na siasa zake za kumpinga papa au mahubiri yake, hatimaye Savonarola alifukuzwa kutoka kanisani, akakamatwa, akateswa ili akiri makosa yake, kisha akanyongwa na kuteketezwa kwa moto.

Maswali Muhimu

Matukio hayo ya kihistoria yanatokeza maswali muhimu. Mbinu na mwenendo wa papa huyo unaweza kufafanuliwaje? Wanahistoria wanasemaje? Wanatoa hoja mbalimbali.

Wengi wanaamini kwamba ili kumwelewa Aleksanda wa Sita, tunapaswa kufikiria kipindi alichoishi. Inadhaniwa kwamba utendaji wake wa kisiasa na wa kidini uliongozwa na tamaa ya kudumisha amani, usawa kati ya majimbo yenye kupingana, kuimarisha uhusiano wa kirafiki pamoja na washirika ambao wangetetea utawala wa kipapa, na kuunganisha utawala wa Jumuiya ya Wakristo dhidi ya tisho la Waturuki.

Namna gani mwenendo wake? Msomi mmoja anasema hivi: “Katika enzi zote za Kanisa kumekuwa na Wakristo wabaya na makasisi wasiofaa. Ili yeyote asishangazwe na jambo hilo, Kristo mwenyewe alilitabiri; hata alilinganisha Kanisa lake na shamba lenye ngano na magugu, au wavu wenye samaki wazuri na wabaya, kama vile alivyomvumilia Yuda kati ya mitume wake.” *

Msomi huyohuyo aliendelea kusema: “Kama vile kitu cha pambo kilichoharibika hakipunguzi thamani ya kito, ndivyo dhambi za kasisi zisivyoweza kuharibu . . . mambo anayofundisha. . . . Dhahabu inabaki dhahabu, iwe inatolewa na mikono iliyo safi au isiyo safi.” Mwanahistoria mmoja Mkatoliki anatoa hoja kwamba kiwango ambacho Wakatoliki wanyofu walipaswa kufuata kuhusu kisa cha Aleksanda wa Sita kinapatikana katika shauri ambalo Yesu aliwapa wanafunzi wake kuhusu waandishi na Mafarisayo: ‘Fanyeni kama wasemavyo, lakini msifanye kama watendavyo.’ (Mathayo 23:2, 3) Hata hivyo, je, hoja hizo zinakusadikisha?

Je, Huu Ni Ukristo wa Kweli?

Yesu alitoa mwongozo rahisi wa sifa zinazothibitisha wale wanaodai kuwa Wakristo: “Kwa matunda yao mtawatambua. Watu hawakusanyi kamwe zabibu kutoka kwenye miiba au tini kutoka kwenye michongoma, je, hukusanya? Hivyohivyo kila mti mwema hutokeza matunda bora, lakini kila mti uliooza hutokeza matunda yasiyofaa kitu; mti mwema hauwezi kuzaa matunda yasiyofaa kitu, wala mti uliooza hauwezi kutokeza matunda bora. Basi, kwa kweli kwa matunda yao mtawatambua watu hao.”—Mathayo 7:16-18, 20.

Kwa ujumla, kwa karne nyingi viongozi wa kidini wametimizaje viwango vinavyohitajiwa, na leo wanafuataje kielelezo kilichowekwa na Yesu cha Ukristo wa kweli na ambacho kilifuatwa na wafuasi wake wa kweli? Na tuchunguze maeneo mawili tu—kujiingiza katika siasa na mtindo wa maisha.

Yesu hakuwa mtawala wa ulimwengu. Aliishi maisha sahili sana hivi kwamba alisema ya kuwa hakuwa hata na mahali “pa kulaza kichwa chake.” Ufalme wake haukuwa “sehemu ya ulimwengu,” nao wanafunzi wake hawakupaswa kuwa “sehemu ya ulimwengu kama vile [yeye hakuwa] sehemu ya ulimwengu.” Kwa hiyo Yesu alikataa kujiingiza katika siasa za wakati wake.—Mathayo 8:20; Yohana 6:15; 17:16; 18:36.

Hata hivyo, je, si kweli kwamba kwa karne nyingi dini mbalimbali zimekuwa zikishirikiana na watawala wa kisiasa kwa ukawaida ili kupata mamlaka na faida za kimwili, ingawa jambo hilo limefanya watu wa kawaida wateseke? Je, si kweli pia kwamba wengi wa makasisi wa dini hizo huishi maisha ya raha ingawa waumini wao wengi ambao wanapaswa kuhudumiwa wanaishi katika umaskini?

Yakobo, ndugu wa kambo wa Yesu alisema: “Wanawake wazinzi, je, hamjui kwamba urafiki na ulimwengu ni uadui na Mungu? Kwa hiyo, yeyote yule atakaye kuwa rafiki ya ulimwengu anajifanya mwenyewe kuwa adui ya Mungu.” (Yakobo 4:4) Kwa nini “adui ya Mungu”? Andiko la 1 Yohana 5:19 linasema hivi: “Ulimwengu mzima unakaa katika nguvu ya mwovu.”

Kuhusiana na maadili ya Aleksanda wa Sita, mwanahistoria mmoja aliyeishi siku za Borgia aliandika hivi: “Mtindo wake wa maisha ulikuwa mpotovu. Hakuwa na aibu, unyofu, imani wala dini. Alikuwa mwenye pupa nyingi, mwenye kujitakia makuu kupita kiasi, mwenye ukatili wa kinyama, na tamaa kubwa ya kufanya watoto wake wengi wawe watu mashuhuri.” Bila shaka, Borgia hakuwa mshiriki pekee mwenye cheo cha kidini aliyetenda hivyo.

Maandiko husema nini kuhusu mwenendo huo? Mtume Paulo aliuliza hivi: “Ama! Je, hamjui kwamba watu wasio waadilifu hawatarithi ufalme wa Mungu? Msiongozwe vibaya. Wala waasherati . . . wala wazinzi, wala . . . watu wenye pupa. . . hawatarithi ufalme wa Mungu.”—1 Wakorintho 6:9, 10.

Mojawapo ya makusudi ya maonyesho yaliyofanywa hivi karibuni huko Roma kuhusu familia ya Borgia lilikuwa “kuwaelewa watu hao mashuhuri kwa kufikiria wakati walioishi . . . , ili kuelewa bali si kuwasamehe wala kuwashutumu.” Kwa kweli, wageni walikuwa na uhuru wa kufikia mkataa wowote. Kwa hiyo, wewe umefikia mkataa gani?

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 20 Kwa maelezo sahihi kuhusu mifano hiyo, ona Mnara wa Mlinzi, Februari 1, 1995, ukurasa wa 5-6, na Juni 15, 1992, ukurasa wa 17-22.

[Picha katika ukurasa wa 26]

Rodrigo Borgia, Papa Aleksanda wa Sita

[Picha katika ukurasa wa 27]

Borgia alimtumia binti yake Lucrezia, kuzidisha mamlaka yake

[Picha katika ukurasa wa 28]

Cesare Borgia alikuwa mtu mwenye kujitakia makuu na mfisadi

[Picha katika ukurasa wa 29]

Kwa kuwa Girolamo Savonarola hakuweza kunyamazishwa, alinyongwa na kuteketezwa kwa moto