Hamia kwenye habari

Awamu ya 3 ya Picha za Warwick (Januari Hadi Aprili 2015)

Awamu ya 3 ya Picha za Warwick (Januari Hadi Aprili 2015)

Katika mfululizo huu wa picha, ona maendeleo ya ujenzi wa makao makuu mapya ya Mashahidi wa Yehova kati ya mwezi wa Januari hadi Aprili 2015.

 

  1. Jengo la Gereji

  2. Jengo la Maegesho ya Magari ya Wageni

  3. Jengo la Udumishaji na Maegesho ya Wenyeji

  4. Jengo la Makazi B

  5. Jengo la Makazi D

  6. Jengo la Makazi C

  7. Jengo la Makazi A

  8. Jengo la Ofisi na Huduma Mbalimbali

Januari 2, 2015​—Jengo la Gereji

Harold Corkern, msaidizi wa Halmashauri ya Utangazaji ya Baraza Linaloongoza, akitoa hotuba ya Kimaandiko yenye kichwa “Jitahidi Kufikia Uwezo Wako.” Mara kwa mara wasemaji mbalimbali hutembelea eneo la ujenzi la Warwick ili kuwatia moyo wajitoleaji

Januari 14, 2015​—Jengo la Ofisi na Huduma Mbalimbali

Turubai jeupe la plastiki linalowasaidia wafanyakazi kuendelea na shughuli zao wakati wa baridi kali. Sehemu hii ya jengo itatia ndani chumba cha kulia chakula, zahanati, jiko, na dobi.

Januari 16, 2015​—Jengo la Makazi D

Fundi umeme wakiandaa nyaya ili kuziunganisha. Zaidi ya mita 12,000 tayari zimefungwa katika majengo ya makazi. Kazi ya kuunganisha nyaya za umeme ilianza tangu eneo liliponunuliwa na itaendelea hadi ujenzi utakapokamilika.

Januari 16, 2015​—Jengo la Makazi A

Mjenzi akifunika roshani kwa karatasi yenye gundi ikiwa ni moja kati ya hatua za kuzuia maji yasipenye. Vibaraza vya ghorofa ya juu kabisa hupakwa polymethyl methacrylate (PMMA)​—kemikali isiyopitisha maji.

Januari 23, 2015​—Jengo la Makazi A

Baba na binti yake wakifunga nyaya za umeme zitakazosambaza umeme katika vyumba.

Februari 6, 2015​—Jengo la Gereji

Wafanyakazi wakila katika chumba cha kulia chakula cha muda. Zaidi ya watu 2,000 hula hapa kila mchana.

Februari 12, 2015​—Jengo la Udumishaji na Maegesho ya Wenyeji

Kikosi cha ujenzi kikifunga vyuma kabla ya kumimina zege kwa ajili ya chumba cha chini ya ardhi kilicho chini ya ofisi za udumishaji.

Februari 12, 2015​—Jengo la Makazi C

Barua kutoka kwa watoto za kuwashukuru wajenzi. Wengi kati ya wafanyakazi hujitolea kwa kipindi kifupi. Wajitoleaji wapya 500 hivi huwasili kila juma. Katika mwezi wa Februari, watu 2,500 hivi walifanya kazi kila siku katika mradi wa ujenzi wa Warwick.

Februari 24, 2015​—Eneo la Ujenzi la Warwick

Karibu asilimia 60 ya mradi wa ujenzi umekamilika. Kati ya Januari na Aprili 2015, majengo ya makazi yalisimamishwa na mhimili wa vyuma wa Jengo la Ofisi na Huduma Mbalimbali ulikamilishwa. Katika kipindi hicho, wajitoleaji walianza kusimamisha kuta za Jengo la Udumishaji, walijenga njia zinazounganisha majengo, na walikarabati bwawa kwenye Ziwa Sterling Forest (Blue Lake).

Februari 25, 2015​—Jengo la Ofisi na Huduma Mbalimbali

Kulitazama jengo kutoka chini. Kampuni ya ujenzi ilipewa kandarasi ya kutengeneza fremu ya jengo hili la ghorofa tano, kisha wajitoleaji Mashahidi wakamwaga saruji.

Februari 26, 2015​—Jengo la Udumishaji na Maegesho ya Wenyeji

Wajenzi wakifunga vyuma kabla ya kumimina zege kwenye sakafu ya ghorofa ya kwanza katika siku yenye baridi. Kati ya miezi ya Januari na Machi, karibu sentimita 127 ya theluji ilianguka eneo la ujenzi la Warwick. Kikosi cha kuondoa theluji kilisafisha eneo hilo na vituo vya kupasha joto viliwasaidia wafanyakazi.

Machi 12, 2015​—Jengo la Maegesho ya Magari ya Wageni

Mabati yakiwekwa katika jengo. Kufikia mwishoni mwa Aprili, sehemu kubwa ya paa za majengo ya makazi ziliezekwa. Kufikia katikati ya mwezi wa Juni paa katika Jengo la Makazi B zitakuwa zimeezekwa.

Machi 18, 2015​—Jengo la Udumishaji na Maegesho ya Wenyeji

Kulitazama Jengo la Makazi B kutoka kwenye kreni.

Machi 18, 2015​—Jengo la Udumishaji na Maegesho ya Wenyeji

Fundi-bomba wakitazama michoro katika Jengo la Gereji. Mradi mzima wa ujenzi unahitaji zaidi ya michoro 3,400 iliyoidhinishwa.

Machi 23, 2015​—Jengo la Ofisi na Huduma Mbalimbali

Wafanyakazi wanaweka turubai la plastiki ili kulinda jengo wakiwa kwenye aina fulani ya lifti inayonyanyuliwa na gari. Programu nyingi za mafunzo zinatolewa ili kuhakikisha lifti na vifaa vingine vinatumiwa kwa usalama. Mafunzo hayo ni kwa ajili ya usalama wa lifti mbalimbali, kujilinda dhidi ya kuanguka, kujifunza mambo ya msingi, matumizi ya vifaa vya kupumulia, jinsi ya kufunga kamba na minyororo kwa usalama, na kutoa ishara.

Machi 30, 2015​—Eneo la Ujenzi la Warwick

Majengo ya makazi yaliyo upande wa magharibi. Kufikia mwishoni mwa mwezi wa Aprili, mifumo ya umeme na mifumo mingine ilikuwa ikiendelea kuwekwa kwenye Majengo ya Makazi A, B na D, yanayoonekana kwenye picha. Kazi ya kusimamisha kuta za ndani, kuweka vigae, na kupaka rangi ilikuwa imeanza katika Jengo la Makazi C (halijaonyeshwa kwenye picha).

Aprili 15, 2015​—Jengo la Makazi B

Wafanyakazi wawili wakiwa kwenye lifti wanapaka rangi inayozuia unyevunyevu kupenya kwenye kuta za nje. Inachukua karibu miezi miwili kumaliza kupaka rangi hizo za kuzuia unyevu katika kila jengo la makazi.

Aprili 27, 2015​—Jengo la Ofisi na Huduma Mbalimbali

Waashi wakijenga ukuta wa mawe ya matale. Sehemu hii ya jengo itakuwa na mapokezi ya mizigo na huduma mbalimbali.

Aprili 30, 2015​—Eneo la Ujenzi la Warwick

Mzamiaji aliyekodiwa akibadilisha valvu ya zamani na kuweka mpya katika ziwa la Blue Lake. Kina cha maji ya ziwa hilo kinaweza kupunguzwa ili kuepuka mafuriko ikiwa kimbunga kitatukia kwa kubonyeza tu kitufe kimoja.