Hamia kwenye habari

JE, NI KAZI YA UBUNI?

Ulimi wa Paka

Ulimi wa Paka

 Paka wa nyumbani wanajulikana sana kwa kujisafisha. Wanaweza kutumia asilimia 24 ya muda wao kujisafisha. Wanafaulu kujisafisha vizuri kwa sababu ya jinsi ulimi wao ulivyobuniwa.

 Fikiria hili: Ulimi wa paka una aina fulani ya miiba 290 inayoitwa papillae. Hiyo ni miiba midogo inayoangalia nyuma na iliyo imara kama ukucha. Kila mwiba una mwanya unaokusanya mate paka anapoingiza ulimi ndani ya mdomo wake. Paka anaporamba manyoya yake, miiba hiyo huingia ndani kabisa ya manyoya hayo na kuruhusu mate yaingie kwenye ngozi.

Papillae iliyokuzwa zaidi

 Ulimi wa paka una uwezo wa kupaka mililita 48 hivi za mate kwenye ngozi na manyoya yake kila siku. Mate hayo huwa na vimeng’enya vinavyoondoa sumu. Kwa kuongezea, mate hayo yanapovukizwa husaidia kupoza mwili wa paka kwa asilimia ishirini na tano, jambo muhimu sana kwa kuwa paka wana tezi chache za kutoa jasho.

 Ikiwa mwiba mmoja katika ulimi wake unanaswa na manyoya, paka huingiza ulimi ndani zaidi ya manyoya na kwa nguvu zaidi na hivyo kuunasua. Pia, ncha za miiba husisimua ngozi ya paka anapojisafisha. Watafiti waliiga ulimi wa paka na kutengeneza brashi ya nywele ya majaribio. Brashi hiyo inachana nywele kwa kutumia nguvu kidogo kuliko brashi ya kawaida na ni rahisi kusafisha kwa kuwa inaachilia nywele zilizojisokota. Watafiti wanaamini kwamba ulimi wa paka unaweza kuwa chanzo cha kubuni kifaa bora kitakachotumiwa kusafisha maeneo yenye nywele na yasiyo na mpangilio. Inaweza pia kutumiwa kuboresha mbinu za kupaka mafuta au dawa juu ya ngozi iliyofunikwa na nywele.

 Una maoni gani? Je, ulimi wa paka ulijitokeza wenyewe? Au ulibuniwa?