Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Gari-Moshi Lisilo na Magurudumu

Gari-Moshi Lisilo na Magurudumu

Gari-Moshi Lisilo na Magurudumu

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI HONG KONG

HATA kabla ya kupanda gari-moshi jipya lenye kung’aa huko Shanghai, China, abiria wanahisi kwamba wanasafiri kwenye reli ya pekee. Hisia hiyo huongezeka gari-moshi hilo linapoondoka kwenye kituo chake cha kisasa kabisa na kusonga kasi na kwa wororo kwa mwendo wa kilomita zaidi ya 430 kwa saa, na hivyo kulifanya gari-moshi la kibiashara linalosonga kwa kasi zaidi duniani. Gari hilo hutumia dakika nane kufika kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Pudong kilicho umbali wa kilomita 30 hivi. Lakini jambo la pekee kuhusu gari-moshi hilo ni kwamba halina magurudumu!

Reli ya kutoka Shanghai hadi Pudong ndiyo reli pekee ulimwenguni ya kibiashara yenye gari-moshi lisilo na magurudumu linaloitwa maglev. Badala ya magurudumu ya chuma, gari-moshi hilo hutegemezwa hasa kwa sumaku. Na badala ya kuendeshwa na mwanadamu, lina tekinolojia inayoonyesha mahali hususa ambapo gari-moshi hilo liko na kuwasilisha habari hiyo kwenye kituo kikuu. Kwenye kituo hicho, watu hutumia kompyuta kuongoza kwa usahihi mwendo wa gari-moshi.

Maglev na Reli za Kawaida

Ujenzi wa gari-moshi hilo la pekee pamoja na reli yake ulitokeza matatizo kadhaa. Kwa mfano, gari-moshi hilo huacha nafasi ndogo tu linapoelea juu ya reli. Kwa kuwa udongo huko Shanghai ni mwororo, wahandisi walilazimika kutumia vifaa vya pekee vya kuunganisha reli hiyo. Vifaa hivyo vinasaidia reli isizame kwenye udongo. Pia, walihitaji kufikiria mabadiliko ambayo hutokea kwenye nguzo za saruji yanayosababishwa na mabadiliko ya kiwango cha joto na kuzifanya nguzo hizo zipanuke au zijikunje.

Hata hivyo, gari-moshi la maglev lina faida nyingi. Kwa mfano, halina kelele zinazosababishwa na mota au magurudumu, na halitoi moshi. Gari-moshi hilo na reli yake hazihitaji kudumishwa mara nyingi. Gari-moshi hilo halitumii nishati nyingi likilinganishwa na magari au ndege za abiria. Kwa kweli, kiwango cha nishati ambacho gari-moshi hilo hutumia ili kuelea ni kidogo kuliko kile kinachotumiwa na mfumo wake wa kusafishia hewa! Kwa kuongezea, tofauti na gari-moshi lenye magurudumu gari-moshi hilo linaweza kupanda milima mikali, kupiga kona kali, na hivyo kupunguza uhitaji wa kuchimba ili kutengeneza reli.

Kwa sababu ya faida hizo zote, inashangaza kwa nini reli nyingi za maglev hazijatengenezwa. Sababu moja ni gharama kubwa inayohusika. Kwa kweli, maofisa nchini China wamesimamisha mpango wa kujenga reli ya maglev kati ya Shanghai na Beijing kwa sababu ujenzi huo ungegharimu mara mbili zaidi ya ujenzi wa reli ya gari-moshi la umeme. Pia, reli ya maglev haiwezi kuunganishwa na reli zilizopo nchini China.

Reli ya maglev huko Shanghai hutumia tekinolojia ya Ujerumani na uchunguzi kuhusu maglev unaendelea nchini Ujerumani, Japani, na katika sehemu nyingine za dunia. Mnamo Desemba (Mwezi wa 12) 2003, gari-moshi la maglev lililotengenezwa nchini Japani liliweka rekodi ya gari-moshi linaloenda mbio zaidi ulimwenguni ya mwendo wa kilomita 581 hivi kwa saa. Kwa sasa, gari-moshi la Shanghai bado ni la pekee kwa ajili ya biashara.

Gari-moshi la maglev linapotoka Pudong kurudi Shanghai, macho ya abiria wote huwa yamekazwa kwenye vipima-mwendo vilivyo katika kila behewa ili waone gari hilo litasonga kwa kasi kadiri gani. Kwa kweli, wanaposafiri mara ya kwanza, abiria wengi hawaoni mandhari vizuri, hivyo wao husafiri tena kwa gari-moshi hilo. Wanapoona ardhi ikisonga kasi sana, wao huelewa kabisa kwa nini maglev limeitwa “ndege isiyo na mabawa.”

[Sanduku/Mchoro katika ukurasa wa 24]

SUMAKU HUENDESHAJE MAGLEV?

Sumaku zinazodhibitiwa kwa vifaa vya elektroniki (1) zinawekwa kwenye sehemu ya chini ya kila behewa, pamoja na sumaku zinazowekwa kwenye sehemu ya chini ya reli (2), huinua gari-moshi hadi sumaku hizo mbili zitenganishwe kwa umbali wa sentimita 2.5 hivi. Sumaku nyingine (3) hufanya gari-moshi hilo lisimame wima. Nyaya fulani za umeme (4) kwenye reli hutokeza msukumo wa sumaku unaosaidia gari-moshi kusonga.

Ili kuhifadhi umeme, kituo kikuu huelekeza nguvu za umeme kwenye sehemu fulani ya reli (5) wakati gari-moshi linapopita mahali hapo. Nguvu nyingi huelekezwa mahali ambapo gari-moshi linastahili kuongeza kasi au kupanda mlima. Gari-moshi linapohitaji kupunguza mwendo au kurudi nyuma, nguvu za sumaku za nyaya za umeme kwenye reli hugeuza mkondo.

JE, NI SALAMA?

Ingawa gari-moshi la maglev husafiri kwa kasi sana, sehemu ya chini ya kila behewa (6) hujishikilia kwa njia fulani kwenye reli na hivyo kufanya isiwe rahisi kuanguka. Si lazima mtu ajifunge mkanda wa usalama, na abiria wanaweza kutembea hata wakati gari-moshi linasonga kwa kasi. Umeme unapopotea, breki fulani za pekee zinazoendeshwa kwa betri hutokeza nguvu za sumaku zinazopunguza mwendo wa gari-moshi kufikia kilomita 10 kwa saa. Kisha gari-moshi huanza kuteleza kwenye reli hadi linaposimama.

Je, sumaku zenye nguvu za gari-moshi hilo ni hatari kwa afya, kwa mfano, kwa abiria walio na vifaa vya kusaidia moyo upige? Imeonekana kwamba hakuna hatari inayotokezwa. Kwa kweli, gari-moshi hilo halina nguvu nyingi za sumaku kwa kulinganishwa na magari-moshi mengine.

[Picha katika ukurasa wa 24, 25]

Zaidi ya kilomita 430 kwa saa!

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 24]

Pages 24 and 25: All photos and diagrams: © Fritz Stoiber Productions/Courtesy Transrapid International GmbH & Co. KG