Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Semi Saba Zenye Hekima

Semi Saba Zenye Hekima

Semi Saba Zenye Hekima

SEMI zilizo hapa chini zimetolewa katika kitabu cha kale kilicho na semi nyingi ambazo zina faida na zinatumika leo. Fikiria jinsi semi hizo zinavyoweza kukusaidia kutumia pesa zako kwa njia ya hekima.

1. “Anayependa fedha hatatosheka na fedha, wala anayependa mali hatatosheka na mapato.” (Mhubiri 5:10) Hayo si maneno ya mtu mwenye wivu ambaye alikuwa maskini. Yaliandikwa na Mfalme Sulemani aliyekuwa mmoja wa watu matajiri zaidi, naye aliyaandika kwa kutegemea mambo yaliyompata na aliyojionea. Matajiri wa leo wamesema maneno kama hayo pia.

2. “Kama tunacho chakula na mavazi, tunapaswa kuridhika navyo. Lakini wale wanaotaka kutajirika huanguka katika majaribu.” (1 Timotheo 6:8, 9, Biblia Habari Njema) Maneno hayo yaliandikwa na mtume Paulo, ambaye aliacha kazi maarufu ili awe mfuasi wa Yesu Kristo. Tofauti na viongozi fulani wa kidini leo, Paulo alikataa kabisa kufaidika kifedha kutoka kwa wale aliowafundisha au rafiki zake. Badala yake, alisema hivi kwa unyoofu: “Sikutamani fedha au dhahabu au vazi la mtu. Ninyi wenyewe mnajua kwamba mikono hii imehudumia mahitaji yangu na ya wale walio pamoja nami.”—Matendo 20:33, 34.

3. “Ni nani kati yenu anayetaka kujenga mnara ambaye haketi kwanza na kuhesabu gharama, ili aone kama ana kiasi cha kutosha kuukamilisha?” (Luka 14:28) Mfano huo wa Yesu unaweza kutumiwa katika hali fulani unayoweza kukabili: Unapotaka kununua kitu, hasa unapotumia kadi ya mkopo, je, utanunua vitu ambavyo hukupangia au utakuwa na subira na kuhesabu gharama? Je, kweli unahitaji kitu unachotaka kununua, na unaweza kukigharimia?

4. “Mkopaji ni mtumwa wa mkopeshaji.” (Methali 22:7, BHN) Kuporomoka kwa uchumi ambako kulitokea hivi karibuni kumeonyesha wazi madhara ya kutumia kadi za mikopo na kurundika madeni kwa njia nyingine. “Ni jambo la kawaida kwa mtu leo kuwa na deni la kadi ya mkopo la dola 9,000 au zaidi kwenye kadi kama nne hivi za mkopo,” anasema Michael Wagner katika kitabu chake Your Money, Day One cha mwaka wa 2009.

5. “Mwovu anakopa lakini halipi, lakini mwadilifu anaonyesha kibali na anatoa zawadi.” (Zaburi 37:21) Watu fulani huona kwamba kusema wamefilisika ni njia rahisi ya kutolipa pesa wanazodaiwa. Lakini wale wanaothamini uhusiano wao mzuri pamoja na Mungu, wanaongozwa na dhamiri kulipa madeni ikiwa wanaweza kufanya hivyo, nao pia hutumia mali zao kwa ukarimu.

6. “Nilikuwa kijana, pia nimezeeka, na bado sijamwona mtu yeyote mwadilifu akiwa ameachwa kabisa, wala uzao wake ukitafuta mkate.” (Zaburi 37:25) Maneno hayo yaliandikwa na mtu aliyetendewa kwa njia isiyo ya haki. Kwa miaka mingi alikuwa mkimbizi, nyakati nyingine aliishi katika mapango na nyakati nyingine alikimbilia nchi jirani. Mwishowe, mkimbizi huyo, Daudi, akawa mfalme wa Israeli la kale. Maishani mwake alijionea ukweli wa maneno hayo yaliyotajwa.

7. “Kuna furaha zaidi katika kutoa kuliko ilivyo katika kupokea.” (Matendo 20:35) Maneno hayo yalisemwa na yule mtu mkuu zaidi aliyepata kuishi. “Kwa ajili ya shangwe iliyowekwa mbele yake,” Yesu alitumia maisha yake duniani kuwatumikia wengine. Sasa akiwa kiumbe wa roho asiyeweza kufa, anafurahia uhai mbinguni akiwa kwenye mkono wa kulia wa yule “Mungu mwenye furaha,” Yehova.—Waebrania 12:2; 1 Timotheo 1:11.

Kusudi kubwa zaidi maishani mwetu ni kuiga mfano wa Yesu kwa kufanya yote tunayoweza ili kuwatumikia wengine. Bila shaka utakubali kwamba ni afadhali mtu awe makini kuweka pesa akiba ili aweze kuwapa wengine vitu kwa ukarimu, badala ya kutumia pesa kwa ubinafsi.