Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

SURA YA 99

Yesu Awaponya Wanaume Vipofu, Kisha Amsaidia Zakayo

Yesu Awaponya Wanaume Vipofu, Kisha Amsaidia Zakayo

MATHAYO 20:29-34 MARKO 10:46-52 LUKA 18:35–19:10

  • YESU AWAPONYA WANAUME VIPOFU HUKO YERIKO

  • ZAKAYO MKUSANYA KODI ATUBU

Yesu na wale wanaosafiri pamoja naye wanafika Yeriko, jiji ambalo liko umbali wa siku moja kutoka Yerusalemu. Yeriko ni majiji mawili, jiji la zamani liko kilomita moja na nusu hivi kutoka jiji jipya lililojengwa na Waroma. Yesu na umati wanapotoka katika jiji moja na kuelekea lingine, wanaume wawili vipofu ambao wanaombaomba wanasikia kelele. Mmoja wao anaitwa Bartimayo.

Bartimayo na mwenzake wanaposikia kwamba Yesu anapita hapo karibu, wanasema kwa sauti kubwa: “Bwana, Mwana wa Daudi, tuhurumie!” (Mathayo 20:30) Baadhi ya watu katika umati wanawaambia kwa ukali wanyamaze, lakini wanaume hao wawili wanaendelea kupaza sauti hata zaidi. Yesu anaposikia kelele hizo anasimama. Anawaomba wale walio pamoja naye wamwite yule anayepaza sauti. Wanaenda kwa wale ombaomba na kumwambia mmoja wao: “Jipe moyo! Simama; anakuita.” (Marko 10:49) Akiwa amesisimka, yule kipofu anatupa vazi lake la nje, anasimama mara moja, na kumwendea Yesu.

Yesu anawauliza: “Mnataka niwafanyie nini?” Vipofu wote wawili wanamsihi: “Bwana, tunaomba macho yetu yafunguliwe.” (Mathayo 20:32, 33) Yesu anawahurumia, anagusa macho yao, na kumwambia mmoja wao: “Nenda, imani yako imekuponya.” (Marko 10:52) Ombaomba hao wawili vipofu wanaanza kuona, na bila shaka wanaanza kumsifu Mungu. Watu wanapoona jambo lililotendeka, wao pia wanamsifu Mungu. Wanaume hao waliokuwa vipofu, sasa wanaanza kumfuata Yesu.

Umati mkubwa sana umemzunguka Yesu anapopitia Yeriko. Kila mtu anataka kumwona yule aliyewaponya wanaume waliokuwa vipofu. Watu wanamsonga Yesu kutoka kila upande; wengine hata hawawezi kumwona. Zakayo pia anashindwa kumwona. Zakayo ndiye mkuu wa wakusanya kodi huko Yeriko na maeneo yaliyo karibu. Kwa kuwa ni mfupi, hawezi kuona kinachoendelea. Basi anakimbia mbele na kupanda mti wa mforsadi-tini ulio katika njia ambayo Yesu anapitia. Akiwa hapo juu, Zakayo anaona kila kitu vizuri. Yesu anapokaribia na kumwona Zakayo akiwa juu ya mti anamwambia: “Zakayo, shuka haraka, kwa maana leo lazima nikae nyumbani kwako.” (Luka 19:5) Zakayo anashuka na kwenda nyumbani haraka ili akafanye matayarisho ya kumkaribisha mgeni wake wa pekee.

Watu wanapoona jambo linaloendelea, wanaanza kulalamika. Wanafikiri kwamba ni kosa Yesu kumtembelea mtu wanayemwona kuwa mtenda dhambi. Zakayo amepata utajiri wake kwa njia isiyo ya haki, kwa kutoza pesa nyingi zaidi anapokusanya kodi.

Yesu anapoingia nyumbani kwa Zakayo, watu wanalalamika hivi: “Ameenda kumtembelea mtenda dhambi.” Hata hivyo, Yesu anaona kwamba Zakayo ana nia ya kutubu. Na Yesu hakatishwi tamaa. Zakayo anasimama na kumwambia: “Tazama! nitawapa maskini nusu ya mali zangu, Bwana, na chochote nilichomnyang’anya mtu, nitamrudishia mara nne.”—Luka 19:7, 8.

Zakayo anatumia njia nzuri sana kuthibitisha kwamba ametubu kikweli! Huenda anaweza kutumia rekodi zake za kukusanya kodi kufanya hesabu ili kuona kiasi alichopokea kutoka kwa Wayahudi mbalimbali, naye anaapa kuwarudishia mara nne zaidi. Hicho ni kiasi kikubwa kuliko inavyohitajiwa na Sheria ya Mungu. (Kutoka 22:1; Mambo ya Walawi 6:2-5) Isitoshe Zakayo anaahidi kuwapa maskini nusu ya mali yake.

Yesu anafurahi anapoona uthibitisho huo unaoonyesha kwamba Zakayo ametubu naye anamwambia: “Leo wokovu umekuja katika nyumba hii, kwa sababu yeye pia ni mwana wa Abrahamu. Kwa maana Mwana wa binadamu alikuja kutafuta na kuokoa kilichopotea.”—Luka 19:9, 10.

Hivi karibuni, Yesu alizungumzia hali ya ‘waliopotea’ akitumia mfano wa mwana mpotevu. (Luka 15:11-24) Sasa ameonyesha mfano halisi wa mtu aliyekuwa amepotea lakini amepatikana. Viongozi wa kidini na wafuasi wao wanaweza kulalamika kumhusu Yesu na kumshutumu kwa kuwasaidia watu kama Zakayo. Hata hivyo, Yesu anaendelea kuwatafuta na kuwarudisha wana hao wa Abrahamu waliopotea.