Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

JE, NI KAZI YA UBUNI?

Mzunguko wa Maisha ya Nyenje

Mzunguko wa Maisha ya Nyenje

NYENJE ni wadudu wanaofanana na nzige ambao wanapatikana katika mabara yote duniani isipokuwa bara la Antaktika pekee. Hata hivyo, nyenje fulani wanaopatikana kaskazini mashariki mwa Marekani wamewavutia wasomi wa elimu ya viumbe kwa muda mrefu.

Fikiria hili: Mamilioni ya Nyenje hujitokeza ghafla kwa majuma machache katika majira ya kuchipua. Baada ya kupigwa na mwanga wa jua kwa muda mfupi, wanavua magamba yao, wanaimba kwa sauti kubwa, wanaruka, na kuzaliana kisha wanakufa. Jambo la kushangaza ni kwamba, kizazi kinachofuata kitajitokeza baada ya miaka 13 au 17, ikitegemea jamii ya wadudu hao. Ni nini kinachotukia kwa wadudu hao kwa muda huo wote kabla hawajatokea?

Ili kujibu swali hilo, tunahitaji kuelewa mzunguko wa kustaajabisha wa maisha ya wadudu hao. Juma moja hivi baada ya kutoka, wadudu hao hujamiiana, na hutaga mayai kati ya 400 hadi 600 kwenye matawi ya miti. Baada ya hapo nyenje hao hufa. Majuma machache baadaye mayai hujiangua na vitoto huanguka ardhini na kisha wanaingia chini ya ardhi na kuanza maisha huko, ambapo wataishi kwa kufyonza majimaji ya mizizi ya miti au vichaka kwa miaka kadhaa. Miaka 13 au 17 baadaye, kizazi kingine cha wadudu hao hutoka ardhini na kuendeleza tena mzunguko wao wa maisha.

Gazeti liitwalo Nature linaeleza kwamba mzunguko huo wa maisha ya nyenje “umewashangaza wanasayansi kwa muda mrefu. . . . Hata sasa, wasomi wa elimu ya wadudu, wanajaribu kujifunza ili waelewe jinsi mzunguko huo wa pekee wa wadudu hao unavyokuwa.” Huo ni mzunguko wa pekee usioweza kuelezeka.

Una maoni gani? Je, mzunguko wa maisha ya nyenje ulijitokeza wenyewe? Au ulibuniwa?